Mamlaka za usalama wa barabarani nchini Nigeria zimesema kuwa uchunguzi wa awali unaonyesha ajali ya gari iliyomhusisha bingwa wa zamani wa dunia wa uzito wa juu, Anthony Joshua, ilisababishwa na kupasuka kwa tairi pamoja na mwendo wa kasi kupita kiasi.
Kwa mujibu wa Shirika la Udhibiti na Utekelezaji wa Trafiki (TRACE), gari la aina ya SUV ambalo Joshua alikuwa akisafiria lilipatwa na tatizo la tairi ya mbele kabla ya kupoteza mwelekeo na kuligonga lori lililokuwa limesimama kando ya barabara. Ajali hiyo ilitokea Jumatatu asubuhi kwenye barabara kuu inayounganisha miji ya Lagos na Ibadan, kusini-magharibi mwa Nigeria.
Anthony Joshua, mwenye umri wa miaka 36, alinusurika ajali hiyo na alikimbizwa katika Hospitali ya Duchess International mjini Lagos ambako hali yake ilielezwa kuwa thabiti. Hata hivyo, ajali hiyo ilisababisha vifo vya watu wawili waliokuwa washirika wake wa karibu na wanachama wa timu yake.
Msemaji wa TRACE alisema dalili za awali zinaonyesha kuwa gari lilikuwa likiendeshwa kwa kasi kubwa, hali iliyochangia kupasuka kwa tairi na kusababisha dereva kupoteza udhibiti. Polisi wa Nigeria walithibitisha kuwa vifo vilitokea papo hapo katika eneo la ajali.
Picha na video zilizosambaa mtandaoni zilimuonyesha bondia huyo wa asili ya Uingereza mwenye mizizi ya Nigeria akisaidiwa kutoka kwenye gari lililoharibika vibaya. Joshua anajulikana kutembelea Nigeria mara kwa mara, hasa katika eneo ambalo familia yake inatoka.
CHANZO: TRT Afrika














