Nchi mbalimbali za Afrika zimeipongeza Tanzania kwa mafanikio yake katika kukuza mchango wa sekta ya madini kwenye pato la taifa, zikisema taifa hilo limekuwa mfano wa kuigwa katika usimamizi wa rasilimali madini.
Pongezi hizo zilitolewa wakati wa Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji wa Madini unaofanyika jijini Nairobi, ambapo mawaziri wa madini kutoka mataifa mbalimbali walieleza kuvutiwa na hatua zilizopigwa na Tanzania katika kuifanya sekta hiyo kuwa moja ya nguzo kuu za uchumi.
Waziri wa Madini wa Kenya, Hassan Ali Joho, alisema Tanzania imeonyesha njia sahihi ya kuendeleza sekta ya madini kwa kuunganisha uwekezaji, usimamizi bora na sera madhubuti.
Naye Waziri wa Petroli na Rasilimali Madini wa Somalia, Dahir Shire Mohamed, alisema Somalia inataka kujifunza kutoka Tanzania ili kuboresha mifumo yake ya usimamizi wa rasilimali za madini.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini wa Tanzania Anthony Mavunde alisema mafanikio hayo yametokana na mageuzi ya kisera na mazingira bora ya uwekezaji yaliyoanzishwa na serikali.














