Afrika

AU yaridhishwa na hatua ya kusitishwa mapigano Jamhuri ya Afrika ya Kati

Umoja wa Afrika umetoa wito kwa makundi yenye silaha katika nchi hiyo “kuweka silaha zao chini na kushiriki kwa nia njema katika majadiliano ya kitaifa na maridhiano”.

Newstimehub

Newstimehub

18 Julai, 2025

0078ee5bcd05e30126968a0c1b36fe0d40c9b15df62238de5e61af3f52f699b7

Siku ya Ijumaa Umoja wa Afrika umeeleza kuridhishwa kwake kwa kuvunjwa kwa makundi mawili yenye silaha katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, na kutoa wito kwa makundi mengi kusalimisha silaha pia.

Nchi hiyo imekabiliwa na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe tangu kupata uhuru 1960.

Licha ya makubaliano ya amani 2019 kati ya serikali na makundi ya waasi 14, bado kuna makundi mengine yanayoendelea kupigana na kudai udhibiti wa baadhi ya maeneo katika nchi hiyo.

Mwezi Aprili, serikali ilisaini makubaliano ya amani na makundi mawili makubwa: UPC na 3R.

‘Majadiliano ya kitaifa’

Katika taarifa iliyosambazwa katika mitandao ya kijamii, Mkuu wa Tume ya Umoja wa Afrika Mahmoud Ali Youssouf ameeleza kuridhishwa na kuvunjwa kwa makundi ya UPC na 3R, ambako kulitangazwa Julai 10 na viongozi wake.

Taarifa hiyo imetoa wito kwa makundi yote yenye silaha “kusalimisha silaha zao na kwa nia njema kujumuika katika majadiliano ya kitaifa na maridhiano”.

Mapigano ya wenyewe kwa wenyewe ya hivi karibuni katika Jamhuri ya Afrika ya Kati yalianza zaidi ya muongo mmoja uliopita. Serikali imeweka usalama katika miji mikubwa na machafuko yamepungua katika miaka ya hivi karibuni.

Lakini mapigano yanazuka mara kwa mara katika maeneo yaliyo mbali na miji kati ya waasi na jeshi la taifa.