Serikali ya Marekani imetangaza kuanza upitiaji wa kesi za uraia zinazohusisha raia wa Marekani wenye asili ya Somalia, kwa lengo la kubaini iwapo uraia huo ulipatikana kwa njia za udanganyifu zinazoweza kusababisha kubatilishwa kwake.
Kwa mujibu wa Wizara ya Usalama wa Ndani, sheria za uhamiaji za Marekani zinaruhusu serikali kuvua uraia endapo itabainika kuwa mtu aliupata kwa kutoa taarifa za uongo au kwa udanganyifu. Maafisa wanasema uchunguzi huo ni sehemu ya juhudi pana za kuimarisha utekelezaji wa sheria za uhamiaji.
Ingawa kesi za kubatilisha uraia ni nadra na huchukua muda mrefu kusikilizwa, utawala wa Trump umechukua msimamo mkali zaidi tangu kuingia madarakani, ukilenga kuwafukuza wahamiaji, kubatilisha baadhi ya viza na hadhi za ukaazi, pamoja na kufanya uchunguzi wa historia za wahamiaji ikiwemo matumizi ya mitandao ya kijamii.
Katika wiki za hivi karibuni, mamlaka za usalama zimeelekeza macho yao kwa jamii ya Wasomali katika jimbo la Minnesota, zikihusisha baadhi yao na tuhuma za mitandao ya ulaghai inayodaiwa kutumia vibaya mamilioni ya dola za misaada ya kijamii ya serikali.
Hatua hizo zimekosolewa na mashirika ya haki za binadamu na watetezi wa wahamiaji, wanaodai kuwa uchunguzi huo unawalenga Wasomali kwa misingi ya kikabila. Serikali, hata hivyo, inasisitiza kuwa inalenga kulinda usalama wa taifa na kuhakikisha fedha za umma hazitumiki vibaya.
Wakati huo huo, Wizara ya Afya na Huduma za Kijamii ya Marekani imesitisha kwa muda baadhi ya malipo ya misaada ya malezi ya watoto kwa jimbo la Minnesota, ikisema kuwa uthibitisho mkali wa nyaraka na ushahidi wa picha sasa utahitajika kabla ya fedha hizo kutolewa. Serikali ya jimbo hilo imekosoa hatua hiyo, ikisema inaleta siasa katika suala la kijamii na kuwaathiri walengwa wa misaada.
CHANZO: TRT Afrika














