Mjadala mkubwa umeibuka nchini Kenya baada ya Seneti kupokea Mswada wa Marekebisho ya Katiba ya mwaka 2026 unaopendekeza kuwazuia magavana wa zamani kuwania viti vya Mbunge au Mwakilishi wa Kaunti kwa kipindi cha miaka mitano baada ya kuondoka madarakani.
Kwa mujibu wa wabunge waliowasilisha pendekezo hilo, hatua hiyo inalenga kuweka kile kinachoitwa “kipindi cha mapumziko” kwa viongozi hao ili kuruhusu ukaguzi wa matumizi yao ya madaraka kukamilika bila ushawishi wa kisiasa.
Ikiwa sheria hiyo itapitishwa, magavana wa zamani wataruhusiwa kuwania tu nafasi za juu kama urais au makamu wa rais katika kipindi hicho cha miaka mitano.
Mswada huo tayari umepelekwa kwa Kamati ya Kudumu ya Haki, Masuala ya Kisheria na Haki za Kibinadamu kwa uchambuzi zaidi huku ushiriki wa umma ukiendelea hadi Mei 8.














