Nigeria imepata Inspekta Jenerali mpya wa Polisi baada ya Kayode Egbetokun kujiuzulu kwa sababu za kifamilia. Rais Bola Tinubu alimtangaza Tunji Disu kama Kaimu Inspekta Jenerali wa Polisi Jumanne usiku. Hatua inayofuata ni Baraza la Polisi na Seneti kuthibitisha rasmi uteuzi wake.
Disu, aliyezaliwa mwaka 1966, amewahi kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya jeshi la polisi. Aliongoza Idara ya Uchunguzi wa Makosa (FCID) Lagos, akawa Kamishna wa Polisi katika Jimbo la Rivers na pia Abuja (FCT). Pia aliwahi kuongoza kikosi cha kupambana na utekaji nyara na kushiriki operesheni ya Umoja wa Afrika Sudan mwaka 2005–2006.
Uteuzi wake unakuja wakati Nigeria inakabiliwa na hali ngumu ya usalama: mashambulizi ya Boko Haram na Daesh kaskazini-mashariki, magenge ya utekaji nyara kaskazini-magharibi, na uhalifu wa mijini unaochochewa na changamoto za kiuchumi na ukosefu wa ajira. Polisi wamekuwa wakishambuliwa moja kwa moja katika baadhi ya maeneo, jambo linaloonyesha uzito wa jukumu analochukua Disu.
Kwa sasa, macho yote yameelekezwa kwake ili kuona kama ataweza kuimarisha usalama na kurejesha imani ya wananchi kwa vyombo vya dola.
CHANZO: TRT Afrika














