Uganda imeipa leseni kampuni ya Elon Musk ya Starlink, kuanza kutoa huduma ya intaneti nchini humo, Rais Yoweri Museveni wa Uganda alisema katika ujumbe wake kwenye mtandao wa X siku ya Ijumaa.
Kampuni ya Starlink, ambayo ni sehemu ya SpaceX, imekuwa ikipanuka kwa kasi barani Afrika na tayari inatoa huduma zakei katika zaidi ya nchi kumi na mbili, ikiwemo Somalia.
Museveni alisema ameongoza kikao cha kusainiwa kwa “makubaliano ya leseni ya uendeshaji kati ya Tume ya Mawasiliano ya Uganda na Starlink, jambo linaloweka hatua muhimu kuelekea kuanza kwa huduma zao nchini Uganda.”
Tume ya Mawasiliano ya Uganda ndiyo mdhibiti wa sekta ya mawasiliano nchini humo.
“Nimefurahi kwamba Starlink imekubali kufuata sheria na masharti ya Uganda wakati inajiandaa kuanza kutoa huduma nchini,” aliongeza.
Watumiaji wa Uganda kwa muda mrefu wamekuwa wakilalamikia gharama kubwa na kutokuwa na uhakika kwa huduma za intaneti za ndani, hali ambayo baadhi ya watu wanailaani kwa sababu ya ushindani mdogo sokoni.
Kampuni kubwa ya mawasiliano ya Afrika Kusini, MTN Group, ndiyo inayoongoza soko la data Uganda, ikishindana hasa na kampuni tanzu ya Airtel ya India.
















