Serikali ya Tanzania imetangaza kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na Marekani katika sekta ya madini, hususan yale yanayohitajika kwa teknolojia za kisasa kama betri za magari ya umeme na nishati mbadala. Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, alisema utafiti wa kina utafanyika katika leseni za Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), hasa katika mikoa ya Lindi na Mtwara yenye viashiria vikubwa vya madini ya kinye (graphite).
Mavunde alibainisha kuwa mahitaji ya graphite duniani yanatarajiwa kufikia tani milioni 4.5 kwa mwaka ifikapo 2050, jambo linaloiweka Tanzania katika nafasi ya kuwa miongoni mwa wasambazaji wakuu wa madini hayo. Ushirikiano huu pia unalenga kuwajengea uwezo wataalamu wa ndani kupitia mafunzo ya teknolojia za kisasa.
Kwa upande wake, Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Andrew Lentz, alisema Marekani itaendelea kushirikiana na Tanzania kuongeza thamani ya rasilimali, kuvutia uwekezaji na kuchangia uchumi endelevu.
CHANZO: TRT Afrika














