Wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya Afrika Mashariki (EAC) wanatarajia kukutana mkoani Arusha, kwa ajili ya Mkutano wao wa 25, unaotarajiwa kufanyika Machi 7, 2026.
Kulingana na Katibu Mkuu wa EAC Veronica Nduva, mkutano huo wa siku moja, unawaleta pamoja viongozi wa kutoka nchi wanachama 8 ndani ya jumuiya hiyo yenye makao makuu yake jijini Arusha, kujadiliana masuala mbalimbali, yakiwemo mustakabali wa jumuiya hiyo na utekelezwaji wa miradi mbalimbali inayolenga kuboresha maisha ya wananchi wa Afrika Mashariki.
Hali kadhalika, wakati wa mkutano hao, wakuu hao wa nchi watapokea na kujadili; ripoti ya Mwaka ya Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kipindi cha tarehe 30 Novemba 2024 hadi 30 Disemba 2025, ripoti ya Baraza la Mawaziri wa Jumuiya kuhusu Utekelezaji wa Maamuzi na Maelekezo ya Mikutano iliyopita ya Wakuu wa Nchi za EAC, uzinduzi wa Mkakati wa Saba wa Maendeleo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (2026/27 – 2030/31) na uzinduzi wa Dhamana ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC Customs Bond/Guarantee).
Vilevile, mkutano huo utajadili kuhusu; zoezi la kuridhia na kusaini kwa Miswada ya Sheria zilizopitishwa na Bunge la Afrika Mashariki, uteuzi wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kuhuisha Mkataba wa Uteuzi wa Naibu Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, uteuzi wa Majaji wa Mahakama ya Jumuiya na utoaji wa zawadi kwa Washindi wa Uandikaji wa Insha.
Nduva alisisitiza umuhimu wa mkutano huo katika kufanya maamuzi sahihi kwa mustakabali wa jumuiya.
“Ni mkutano muhimu sana katika kusukuma mbele ajenda ya utangamano wa Afrika Mashariki,” alisema Katibu Mkuu huyo anayemaliza muda wake.
Jumuiya ya Afrika Mashariki ina nchi wanachama nane, ikiwa na idadi ya zaidi ya watu milioni 300 na pato la pamoja linalokadiriwa kuzidi dola za Marekani bilioni 300, hali inayoifanya Jumuiya hiyo kuwa miongoni mwa Jumuiya za kikanda zenye soko kubwa na fursa lukuki za uwekezaji barani Afrika.














