Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuidhinisha kwa mara ya kwanza dawa maalum ya kutibu malaria kwa watoto wachanga na watoto wadogo kabisa.
Dawa hiyo ya artéméther-luméfantrine ndiyo tiba ya kwanza ya malaria iliyoundwa mahsusi kwa watoto wachanga, tofauti na dawa zilizokuwa zikitumika hapo awali ambazo zilitengenezwa kwa watoto wakubwa.
WHO imesema kuwa idhini hiyo ya awali ya ubora inaonesha kuwa dawa hiyo inakidhi viwango vya kimataifa vya usalama, ubora na ufanisi.
Hadi sasa, watoto wachanga walikuwa wakitibiwa kwa kutumia dawa za watoto wakubwa, hali iliyoongeza hatari ya makosa ya dozi, madhara na sumu mwilini.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema hatua hiyo inaashiria mabadiliko makubwa katika mapambano dhidi ya malaria, ugonjwa ambao kwa muda mrefu umekuwa ukiua watoto wengi duniani.
















