Ziara ya msanii wa Nigeria Burna Boy nchini Marekani na Canada imeingia katika sintofahamu baada ya maonyesho kadhaa kufutwa ghafla kwa kile Ticketmaster ilichotaja kuwa ni “mauzo duni ya tiketi.” Hata hivyo, wataalamu wa tasnia wanasema kufutwa huko kunatokana na sakata lililotokea kwenye tamasha lake mjini Denver, ambapo alisimamisha shoo kumtoa mwanamke aliyekuwa amelala – baadaye ikathibitika alikuwa katika majonzi. Kauli yake ya mtandaoni kwamba anatafuta “mashabiki wenye pesa” ilichochea hasira zaidi, na baadhi ya mashabiki wakafuta tiketi zao. Tukio hilo limeongeza lawama dhidi ya tabia yake ya jukwaani, na kusababisha shinikizo kubwa la mitandaoni. Kufutwa kwa maonyesho ya Minneapolis na Chicago kumeibua wasiwasi kuhusu mustakabali wa ziara yake ya ‘No Sign of Weakness,’ iliyopangwa kumalizika Desemba 11, 2025.
CHANZO: TRT Afrika









