Waziri Mkuu wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, ametoa wito kwa wizara zinazohusika na masuala ya ajira kusimamia kwa umakini utekelezaji wa sheria zinazolinda nafasi za kazi kwa Watanzania. Amesisitiza kuwa ajira ambazo zinaweza kufanywa na wazawa hazipaswi kutwaliwa na wageni, isipokuwa pale ambapo kuna uhaba wa utaalamu maalum nchini.
Akizungumza Januari 14, 2026, wakati wa kikao cha mawaziri na makatibu wakuu wa wizara za kisekta, Dkt. Nchemba alisema hatua hiyo ni muhimu katika kulinda maslahi ya wananchi na kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira. Alionya dhidi ya tabia ya kuruhusu wageni kufanya kazi ambazo Watanzania wana uwezo wa kuzifanya.
Aidha, Waziri Mkuu alikosoa mwenendo wa baadhi ya wamiliki wa nyumba kuwapangisha raia wa kigeni na kuruhusu makazi hayo kutumika na watu wengi, akieleza kuwa hali hiyo ni tishio kwa usalama wa taifa na inawakosesha Watanzania faida za kiuchumi. Alisisitiza uzalendo na “wivu wa nchi” katika kulinda rasilimali na fursa zilizopo.
Dkt. Nchemba pia alizitaka wizara husika kusimamia kwa makini usajili wa kampuni za kigeni, akibainisha kuwa baadhi ya taarifa zinazowasilishwa hazilingani na uhalisia. Alisema sheria zilizopo zinalenga kukuza kampuni za Watanzania na kuhakikisha uwekezaji wa kigeni unazingatia maslahi ya taifa. Hata hivyo, alisisitiza kuwa Tanzania itaendelea kuwakaribisha wawekezaji wanaofuata sheria na kuchangia maendeleo endelevu ya nchi.
CHANZO: TRT Afrika














