Wakazi wa Khartoum nchini Sudan wanakabiliwa na hatari kubwa kutokana na mabomu ya ardhini ambayo hayajalipuka, yaliyosalia baada ya mapigano makali kati ya vikosi vya kijeshi.
Ripoti zinaonyesha kuwa mabomu hayo yameachwa katika maeneo ya makazi, barabara na hata karibu na shule, jambo linaloweka maisha ya raia hatarini kila siku, Watu wengi wamelazimika kuhama makazi yao kwa hofu ya kulipuka kwa mabomu hayo.
Mashirika ya kibinadamu yameonya kuwa ukosefu wa vifaa na wataalamu wa kusafisha mabomu unafanya hali kuwa mbaya zaidi. Watoto wameonekana kuwa katika hatari kubwa kwani mara nyingi hawatambui hatari ya vitu hivyo wanapocheza.
Mamlaka pamoja na mashirika ya kimataifa yanaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu tahadhari za usalama, huku juhudi za kuondoa mabomu hayo zikiendelea polepole.
Wachambuzi wanasema kuwa tatizo hilo linaweza kuendelea kwa miaka mingi kama hatua za haraka hazitachukuliwa, na linaweza kuzuia kurejea kwa amani na maendeleo ya kawaida katika mji huo.
Chanzo:Africanews














