Waziri wa Madini nchini Tanzania, Anthony Mavunde, amesema sekta ya madini imeendelea kuimarika na sasa imefikia mchango wa asilimia 11.9 katika pato la taifa kutokana na ongezeko la uwekezaji.
Akizungumza Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Mavunde alisema mchango wa sekta hiyo umeongezeka kwa kasi kutoka asilimia 9.1 mwaka 2023 hadi asilimia 10.1 mwaka 2024.
Aliongeza kuwa kufikia robo ya tatu ya mwaka 2025, sekta hiyo ilikuwa tayari imefikia wastani wa mchango wa asilimia 11.9 katika pato la taifa.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, mafanikio hayo yanatokana na kuongezeka kwa uwekezaji na mageuzi yanayoendelea katika sekta ya madini nchini.














